Ozoni

Ozoni (kutoka Kiingereza: ozone, pia trioxygen) ni molekuli yenye alama ya O3 inayofanywa na atomi tatu za oksijeni.
Tabia
Inaonekana kama gesi ya buluu yenye harufu kali. Inatokea katika matabaka ya juu ya angahewa ambako mnururisho wa urujuanimno unapasua molekuli za O2.
Inatokea pia katika mazingira ya mashine kama ya fotokopi zinazotumia volteji ya juu.
Si molekuli thabiti, hivyo inasambaratika tena baada ya muda.
Tabaka la ozoni
Ozoni hupatikana kwa viwango vidogo vya ppm 0.6 katika angahewa. Kiasi kikubwa kipo kwenye tabakastrato baina ya kilomita 10 hadi 50 juu ya uso wa ardhi. Tabaka hili lenye ozoni linafyonza asilimia kubwa ya mnururisho wa urujuanimno (93-99%) ulio hatari kwa viumbehai duniani.
Athari kwa viumbehai
Katika matabaka ya chini ya angahewa ozoni ni sumu kwa viumbehai ikitokea kwa viwango juu ya ppm 0.1. Kwa binadamu inaweza kukera pua na koo pamoja na kuleta kichefuchefu. Kuathiriwa kwa muda mrefu kunaweza kuleta kufura kwa mapafu[1].
Ppm 0.100 ni kiwango cha juu kinachoruhusiwa ndani ya karakana, viwanda au ofisi katika nchi kama Uingereza, Japani, Ufaransa, Uholanzi na Ujerumani.
Matumizi
Kutokana na nguvu yake ya kuoksidisha, ozoni hutumiwa kwa madhumuni mbalimbali:
- kusafisha maji: ozoni inaua bakteria na algae hivyo hutumiwa katika mchakato wa kusafisha maji kwa matumizi ya viwandani na maji ya kunywa
- kuua wadudu katika utunzaji wa vyakula vilivyopikwa, pia kutunza nafaka
- uzalishaji wa madawa: ozoni hutumiwa katika michakato ya kikemia
Marejeo
Kigezo:Marejeo Kigezo:Mbegu-kemia
- ↑ Ozone backround information, Effects on humans, tovuti ya National Center for Biotechnology Information, iliangaliwa Mchi 2019